Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, athari za vita vilivyoilenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaendelea kuonekana katika eneo lote, athari hizo hazijabakia tu katika kiwango cha kijeshi na kisiasa, bali pia zimeenea katika baadhi ya nchi za Ghuba ambazo zimekuwa zikishuhudia hatua kali za kiusalama na kuongezeka kwa mivutano ya ndani.
Nchini Bahrain, wimbi la hivi karibuni la kukamatwa, maamuzi ya kuvuliwa uraia na ufuatiliaji wa kisiasa na kidini limeibua mijadala mikubwa kuhusu hali ambayo nchi hiyo inapitia kwa sasa, hali hii inajitokeza huku mamlaka zikishutumiwa kwa kutumia mazingira ya kikanda kuongeza udhibiti wa kiusalama na kuwashambulia wapinzani, hasa miongoni mwa jamii ya Kishia.
Katika muktadha huu, Dkt. Ibrahim Al-Aradi, mkurugenzi wa ofisi ya kisiasa ya Bahrain February 14 Coalition, katika mazungumzo na tovuti ya habari ya Al-Ahed, alisisitiza kwamba; utawala wa Al-Khalifa kwa miaka mingi umefuata sera ya uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo, kwa maoni yake, vita vya hivi karibuni vimetoa fursa ya kupanua sera hiyo na kuigeuza kuwa hatua za moja kwa moja ndani ya Bahrain.
Amebainisha kwamba; nchi hiyo ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza ambazo ardhi na kambi zake za kijeshi zilitumika katika mfumo wa uvamizi dhidi ya Iran, kwa mtazamo wake, utawala unajaribu kusambaza simulizi kwamba; Iran ndiyo chanzo kikuu cha tishio kwa nchi hiyo, ilhali wananchi wa Bahrain wamezuiwa kutoa maoni au kuuliza sababu za ushiriki wa Bahrain katika mkondo huo.
Mamia ya waliokamatwa kwa misingi ya kimadhehebu
Al-Aradi amesema pia kwamba; Bahrain hivi sasa inashuhudia wimbi kubwa la kukamatwa linalowalenga Mashia, ameeleza kuwa makadirio yasiyo rasmi yanaonesha kwamba; tangu hotuba ya Imam Khamenei, mamia ya wananchi wamekamatwa, huku familia nyingi zikikabiliwa na mashinikizo na vitisho ili zisizungumzie hatima ya watoto wao au kukamatwa kunakowakumba.
Ameongeza kuwa; mamlaka za Bahrain zinachukulia mwelekeo wa fikra na wa kidini unaohusishwa na mfumo wa Wilayat al-Faqih kama kosa linalostahili adhabu. Ameashiria kwamba; yeyote anayeshukiwa kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu au kuwa karibu na mwelekeo huo anafuatiliwa, kukamatwa au kutishiwa kuvuliwa uraia.
Pia ameeleza kwamba; kutokana na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na usalama pamoja na kuendelea kwa hatua za adhabu dhidi ya viongozi wa kidini, kijamii na kitamaduni wanaojulikana, hofu imekuwa imetanda miongoni mwa Mashia.
Mjumbe huyo wa muungano wa Februari 14 ameeleza kuwa; hatua za ufuatiliaji hazijawa dhidi ya wanaharakati wa kisiasa pekee, bali pia zimewajumuisha wanazuoni, wahubiri, wasomaji wa kaswida na watu mashuhuri wa kijamii, kwa mtazamo wake, kinachoendelea ni kampeni iliyopangwa ambayo inalenga mazingira yote ya Kishia.
Pia amesema kuwa; utawala unahimiza moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja hotuba za uchochezi wa kimadhehebu, huku Mashia wakikabiliwa na kampeni za kuharibiwa taswira kutokana na imani zao za kidini na misimamo yao ya kisiasa.
Al-Aradi pia amefichua kuwepo kwa mashinikizo dhidi ya wananchi ili waoneshe utii wa kisiasa kwa utawala wa Bahrain na kujitenga na viongozi wa kidini ambao mamlaka zina tofauti nao.
Kwa maoni yake, hatua hizi zinaonesha ukubwa wa mgogoro ambao utawala unakabiliana nao mbele ya sehemu kubwa ya jamii ya Bahrain.
Amesisitiza kuwa; hatua za hivi karibuni za kukamatwa zimeenea katika maeneo na vijiji mbalimbali vya Bahrain, na kwamba mamlaka zinaendelea kuwafuatilia wale wanaodhaniwa kuwa sehemu ya mkondo wa Muqawama au wanaounga mkono Jamhuri ya Kiislamu.
Amebainisha kuwa; juhudi zozote za kuwalenga wafuasi wa Wilayat al-Faqih kwa vitendo ni sawa na kulenga sehemu kubwa ya Mashia wa nchi hiyo.
Maoni yako